Treni ya abiria yapata ajali Kigoma na kujeruhi 70

0
21

Treni ya abiria namba Y14 ikiwa na kichwa cha treni namba 9002, mabehewa 12 ya abiria, behewa moja la vifurushi (parcel) na behewa moja la breki imepata ajali kati ya Stesheni ya Kazuramimba na Uvinza mkoani Kigoma majira ya saa 7.30 usiku wa kuamkia leo.

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema ajali hiyo imetokea baada ya treni hiyo iliyokuwa na abiria 571 ikitokea Kigoma kuelekea Dar es Salaam kuacha njia na kupelekea majeruhi 70, wanawake wakiwa 26 na wanaume 44.

“TRC kwa kushirikiana na Kitengo cha Afya cha Mkoa wa Kigoma walifanikiwa kuwapeleka majeruhi katika hospitali ya wilaya ya Uvinza kwa ajili ya matibabu. Hali za afya za abiria zinaendelea kuimarika, majeruhi 57 tayari wameruhusiwa, nane wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Uvinza, na watano wamehamishiwa katika hospitali ya Maweni kwa ajili ya matibabu,” imeeleza.

Aidha, Shirika hilo limewapa pole majeruhi, na kwamba linaendelea na jitihada za kuwahudumia, huku likiekeza kuwa hakuna taarifa ya vifo vilivyotokana na ajali hiyo.