Trump afuta vibali vya usalama kwa Biden, Kamala na Hillary Clinton

0
16

Rais Donald Trump ameondoa vibali vya usalama na upatikanaji wa taarifa za siri kwa wapinzani wake wa zamani, wakiwemo Kamala Harris, Hillary Clinton, Joe Biden na mtu yeyote kutoka familia ya Biden.

Trump alitangaza Februari kuwa atazuia Biden kupata taarifa za kijasusi, kama kulipiza kisasi kama alivyofanya kwake baada ya shambulio la Januari 6, 2021, katika jengo la Bunge la Marekani.

Wengine waliohusishwa ni waliowahi kuwa na migogoro na Trump, wakiwemo mwanasheria mkuu wa New York, Letitia James, na mwendesha mashtaka wa Manhattan, Alvin Bragg ambao walifungua kesi dhidi yake, mashahidi wawili waliotoa ushahidi katika kesi ya kwanza ya kumfungulia mashtaka Trump mwaka 2019 kuhusu shinikizo alilomwekea Ukraine pamoja na wakili aliyesimamia kesi hiyo.

Wabunge wawili pekee wa Republican waliokuwa kwenye kamati ya uchunguzi wa shambulio la Januari 6, 2021, Liz Cheney na Adam Kinzinger, pia wamejumuishwa kwenye orodha hiyo.