Trump aitaka Apple itengenezee iPhone Marekani au ikumbane na ushuru wa asilimia 25

Rais wa Marekani Donald Trump ameitaka kampuni ya Apple kutengeneza simu zake ndani ya Marekani, la sivyo ikabiliwe na ushuru wa asilimia 25.
Trump amesema tayari amemjulisha Mkurugenzi Mtendaji wa Apple, Tim Cook, kuwa anatarajia iPhone zitakazouzwa Marekani zitengezwe nchini humo, na si nchi nyingine.
“Nimemwambia Tim Cook wa Apple tangu zamani kwamba nataka simu za iPhone zitakazouzwa Marekani zitengenezwe na kujengwa hapa Marekani, si India wala sehemu nyingine yoyote. Kama hilo halitafanyika, Apple italazimika kulipa ushuru wa angalau asilimia 25 kwa Marekani,” amesema.
Kwa miaka ya karibuni, Apple imekuwa ikijaribu kusambaza uzalishaji wake katika nchi mbalimbali. Sehemu ya uzalishaji wa iPhone tayari imehamishiwa India.
Tim Cook alisema anatarajia simu nyingi za iPhone zitakazouzwa Marekani zitatoka India.
