Rais wa Marekani, Donald Trump amemwalika Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kutembelea Ikulu ya White House Februari 4 mwaka huu.
Mwaliko huo umetolewa kupitia barua rasmi kutoka kwa Trump, akimwalika Netanyahu kujadili juhudi za kuleta amani kati ya Israel na majirani zake, pamoja na mikakati ya kukabiliana na maadui wa pamoja wa mataifa hayo mawili.
Hii ni hatua kubwa inayochukuliwa kama upendeleo kwa mshirika wa Marekani licha ya Netanyahu kuwa miongoni mwa viongozi wanaokabiliwa na tuhuma za uhalifu wa kivita kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
“Itakuwa heshima yangu kukukaribisha kama kiongozi wangu wa kwanza wa kigeni katika muhula wangu wa pili,” imesomeka sehemu ya barua hiyo.
Wakati huo huo, Trump ameeleza wasiwasi wake kuhusu mustakabali wa usitishaji mapigano kati ya Israel na Hamas huko Gaza, akisema hana imani kama utazaa matunda.
Chini ya makubaliano ya usitishaji mapigano, pande hizo mbili zinapaswa kuanza mazungumzo ya amani ya muda mrefu, ingawa wengi wana hofu kuwa juhudi hizo zitashindikana na kusababisha kurejea kwa ghasia baada ya miezi 15 ya mapigano makali.