
Rais wa Marekani, Donald Trump anapanga kufuta hadhi ya hifadhi ya muda kwa takriban wakimbizi 240,000 wa Ukraine waliokimbia uvamizi wa Urusi, hali ambayo itawaweka katika hatari ya kufukuzwa haraka nchini Marekani.
Kwa mujibu wa ripoti, hatua hiyo inaweza kutekelezwa mapema mwezi Aprili.
Mpango wa kuondoa ulinzi kwa Waukraine ulikuwa tayari unaendelea hata kabla ya Trump kuzozana hadharani na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, wiki iliyopita.
Hii ni sehemu ya juhudi pana za utawala wa Trump za kuwafuta hadhi ya kisheria zaidi ya wahamiaji milioni 1.8 waliyoruhusiwa kuingia Marekani chini ya mpango wa hifadhi ya muda ya kibinadamu ulioanzishwa wakati wa utawala wa Biden.
Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani (Department of Homeland Security – DHS) huipa nchi hadhi ya Hifadhi ya Muda (Temporary Protected Status – TPS) ikiwa raia wake hawawezi kurudi nyumbani kwao.
Kaimu waziri wa Usalama wa Ndani anaweza kuipa nchi hadhi ya TPS ikiwa inakabiliwa na mzozo wa kijeshi unaoendelea, janga la mazingira, mlipuko wa ugonjwa, au hali nyingine zisizo za kawaida na za muda mfupi.