
Donald Trump amesema anapanga kuwa mkarimu sana kwa China katika mazungumzo yoyote ya kibiashara, na kwamba ushuru wa forodha utapunguzwa endapo mataifa hayo mawili yatafikia makubaliano.
Trump amesema kuwa ushuru wa bidhaa kutoka China utapunguzwa kwa kiwango kikubwa lakini hautafutwa kabisa, baada ya Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent, kusema anatarajia kupungua kwa mvutano katika vita vya kibiashara kati ya mataifa hayo mawili makubwa zaidi kiuchumi duniani.
Trump aliweka ushuru wa forodha wa asilimia 145 kwa bidhaa za China, huku China ikijibu kwa ushuru wa asilimia 125 kwa bidhaa za Marekani, hali iliyosababisha kuyumba kwa masoko ya hisa na hofu ya kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia.
“Tutakuwa wema sana. Wao pia watakuwa wema, na tutaona nini kitatokea. “Lakini hatimaye ni lazima wafanye makubaliano, la sivyo hawataweza kufanya biashara Marekani,” amesema Trump.
Aidha, China ilieleza mapema mwezi huu kuwa inataka hatua kadhaa zichukuliwe na utawala wa Trump hasa kudhibiti kauli za udhalilishaji kutoka kwa baadhi ya mawaziri wake, kabla ya kukubali kushiriki mazungumzo yoyote.