Tuhuma za rushwa zapelekea chaguzi CCM kuahirishwa

0
41

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amesema chama  hicho kimesitisha uchaguzi wa nafasi ya Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Mkoa wa Mbeya kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwemo tuhuma za rushwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 21, 2022 jijini Dodoma Chongolo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Uchaguzi CCM ametangaza pia kusitisha uchaguzi wa nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa mkoa wa Arusha kutokana na tuhuma alizozitaja hapo mwanzo.

“Tukikamilisha uchunguzi tutatoa taarifa na uamuzi wa chama na kuendeleza au kuruhusu mchakato wa uchaguzi kuendelea,” amesema.

Aidha, amesema uchaguzi uliofanyika jana Novemba 20, 2022 Mkoa wa Magharibi Zanzibar, chama kinafanya uchunguzi kutokana na malalamiko ya baadhi ya wagombea na wajumbe wakieleza kuhusiana na mmoja wa wanachama kuchukua sanduku la kura na kwenda nalo kwenye chumba cha kuhesabia kura.

AFRIMMA yamtunuku Rais Samia Tuzo ya uongozi Bora

“Tukijiridhisha lilikuwepo  lengo lingine tutafuta uchaguzi na kurudia upya ili kutenda haki, tukijiridha kwamba lengo lilikuwa ni kupeleka boksi hilo kwa ajili ya kwenda kuhesabu kura, basi tutaruhusu matokeo hayo yaliyotangazwa jana yaendelee kuwa kama yalivyo,” ameongeza.

Hata hivyo ameeleza kuwa uchaguzi unaendelea katika nafasi zingine za uongozi ukiachilia nafasi hizo zilizositishwa.

Send this to a friend