Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekanusha taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba mfumo wa taarifa za uchaguzi unaotumiwa na tume hiyo umeunganishwa na mfumo wa NIDA na chama kimoja cha siasa nchini, ikiwataka Watanzania kupuuza kwani taarifa hiyo haina ukweli wowote.
Hivi karibuni aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole alitoa kauli hiyo kupitia kwenye mitandao ya kijamii na kuzua mijadala.
Tume imeeleza kuwa taarifa hiyo imeenezwa na mtu ambaye hana uelewa na ufahamu kuhusu mfumo wa uchaguzi, na kwamba Daftari la Kudumu la Wapiga Kura halijaunganishwa na mfumo wowote wa Serikali au taasisi binafsi kwa madhumuni ya upigaji kura.
“Mfumo wa upigaji wa kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo hautumii mfumo wa aina yoyote wa kielektroniki. Mfumo wa upigaji kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo hutumia utaratibu wa kawaida (manual),” imesema taarifa hiyo.
Imeongeza kuwa “mfumo wa upigaji kura kwa Tanzania, mtu aliyeandikishwa hufika mwenyewe katika kituo cha kupigia kura na kuonesha kadi yake ya mpiga kura iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambapo jina lake husomwa kwa sauti na msimamizi wa kituo ili kuwawezesha mawakala wa upigaji kura kujiridhisha iwapo mtu huyo yupo katika daftari, baada ya uhakiki huo ndipo mhusika hupewa karatasi za kura ili aendelee na utaratibu wa kupiga kura.
“Aidha, Tume imesema kitambulisho cha Taifa hakitumiki kupiga kura, bali kadi ya mpiga kura pekee iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.






