
Chama cha ACT Wazalendo kimesema kimepokea barua kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikielekeza kuwa Mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama hicho, Luhaga Mpina asifike ofisi za tume kwa ajili ya kurejesha fomu.
Taarifa iliyotolewa na Chama hicho imesema tume imetoa zuio hilo kutokana na kupokea nakala ya barua kutoka kwa msajili wa vyama vya siasa ambayo imetengua uteuzi wake.
“Maamuzi haya sio tu kwamba ni ya aibu bali yanaibua maswali mengi juu ya uadilifu, umakini, uweledi na uhuru wa Tume ambayo imepewa dhamana ya kikatiba kuwa huru katika kusimamia katiba, sheria, kanuni na utaratibu unaongoza usimamizi wa uchaguzi nchini.
Katiba ya Tanzania ya Mwaka 1977, inaweka msimamo na maelekezo katika Ibara ya 74 (7) kuwa katika utekelezaji wa majukumu yake yaliyoainishwa katika ibara 74(6) Tume ya Uchaguzi itakuwa huru na inayojitegemea. Aidha, Ibara ya 74(11) inailinda Tume kutokulazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au Idara yoyote ya Serikali, au maoni ya chama chochote cha siasa,” imesema.
Aidha, chama hicho kimeeleza kuwa sheria haitoi nafasi kwa tume kukataa kupokea fomu au kutomteua mgombea isipokuwa kwa njia ya pingamizi linalowekwa dhidi ya mgombea kwa utaratibu uliopo chini ya kifungu cha 36 na 37 cha sheria na kanuni ya 22 ya Kanuni za Uchaguzi (2025).
“Kwa maana nyengine hakuna kifungu chochote cha Sheria, Katiba au Kanuni kinachotoa mamlaka kwa tume kuzuia mgombea asirudishe fomu iliyotolewa na tume baada ya kukidhi vigezo vya uchukuaji wa fomu,” imeeleza.
Hata hivyo, ACT-Wazalendo imeiomba tume itengue barua ya Mkurugenzi wa Uchaguzi kwa Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo na kuruhu Mpina kurudisha fomu kama alivyopangiwa awali.








