Tume ya uchaguzi yatangaza uchaguzi wa madiwani kwenye Kata 23

0
44

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata 23 za Tanzania Bara utakaofanyika Machi 20, mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Tume hiyo, Kailima Ramadhani imesema tume imepokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kuhusu uwepo wa nafasi wazi za madiwani katika kata hizo, taarifa iliyozingatia matakwa ya kifungu cha 13(1) na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292.

Aidha imeeleza kuwa fomu za uteuzi zitatolewa kuanzia Februari 26 hadi Machi 04, mwaka huu ambapo uteuzi wa wagombea utafanyika Machi 04, 2024 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Machi 05 hadi 19, mwaka huu.

“Tume inatumia nafasi hii kuvikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia katiba, sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi cha uchaguzi huu mdogo,” imesema taarifa hiyo.

Bunge laazimia Serikali kununua ndege nyingine kuwahudumia viongozi

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kata zitakazofanya uchaguzi huo ni Kimbiji (Manispaa ya Kigamboni), Kasingirima (Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Manispaa ya Tabora), Msangani (Halmashauri ya Mji Kibaha), Fukayosi (Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Wilaya ya Kibiti), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga) na Mbingamhalule (Wilaya ya Songea).

Nyingine ni Isebya (Wilaya ya Mbogwe), Kibata (Wilaya ya Kilwa), Mshikamano (Wilayani Musoma), Busegwe (Wilaya ya Butiama), Nkokwa (Wilaya ya Kyela), Kamwene (Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Wilaya ya Sengerema), Mhande (Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Nkasi), Bukundi (Wilaya ya Meatu) Mkuzi (Wilaya ya Muheza) na Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Wilaya ya Mkinga).

Send this to a friend