Tume ya watu 19 yaundwa kuchunguza ubora wa majengo Kariakoo
Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuelekeza majengo yote Kariakoo kufanyiwa ukaguzi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema tayari tume ya watu 19 imeundwa ili kujua ubora wa majengo pamoja na shughuli zinazoendelea katia eneo hilo.
Akizungumza leo wakati wa kuaga miili ya watu waliofariki baada ya jengo kuporomoko eneo la Kariakoo Novemba 16, 2024, amesema tume hiyo itakayoongozwa na Bregedia Jenerali Hosea Ndagala ambaye ni Mkuu wa Idara ya Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, itaisadia kuishauri Serikali kujua ni hatua gani ifanye baada ya uchunguzi huo.
“Mahitaji ya Soko la Kariakoo bado yako palepale. Soko la Kariakoo ni soko la kimataifa kwa sasa linalotegemewa na nchi zote zinazotuzunguka hapa jirani, kwahiyo tunayo sababu ya kuimarisha lakini pia kutambua ubora wa majengo tuliyonayo,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema mpaka sasa idadi ya vifo ni 16 na majeruhi ni 86 ambapo wengi wameruhusiwa na watano wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali nchini.
Mbali na hayo, amewataka Watanzania kutotumia maafa yanayotokea katika jamii kama fursa ya kujifaidisha, huku akionya kuwa mtu yeyote haruhusiwi kuchangisha michango ya kusaidia operesheni ya uokozi isipokuwa akaunti maalum ya maafa iliyoko Benki Kuu (BoT), yenye jina la National Relief Fund kwa namba 9921159801.
Hata hivyo, ameliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta mmiliki wa jengo lililoanguka ili kulisaidia Jeshi la Polisi na kujua sababu za jengo hilo kuanguka.