Tume yasisitiza ACT- Wazalendo haina mgombea Urais

0
125

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesisitiza kuwa Chama cha ACT-Wazalendo hakina wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, hivyo taarifa ya chama hicho inayoeleza uwepo wa wagombea wa nafasi hizo, si sahihi.

Taarifa iliyotolewa Septemba 21, 2025 katika tovuti ya chama hicho imeonesha uwepo wa mkutano wa uzinduzi wa ilani ya uchaguzi katika makao makuu ya chama hicho na kufuatiwa na uzinduzi wa kampeni za ubunge katika jimbo la Segerea.

Katika taarifa hiyo imebainisha kuwa shughuli zote mbili zitahudhuriwa na waliotajwa kama wagombea wa kiti cha Rais, Luhaga Mpina na Makamu wake, Fatma Ferej. Hata hivyo Tume imeeleza kuwa uamuzi wa Tume wa Septemba 15, 2025 ulitengua uteuzi wa Mpina na kwamba waliokuwa wagombea wa nafasi hizo walijulishwa kwa barua kuhusu uamuzi huo wa Tume.

Aidha, imeeleza kuwa taarifa ya msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Segerea, ambaye ndiye mratibu wa ratiba za kampeni za Ubunge, inaonesha kuwa hakuna ratiba ya kampeni za mgombea ubunge wa chama cha ACT Wazalendo katika eneo lililotajwa katika taarifa ya chama hicho.

INEC imeshauri na kusisitiza kuwa Chama cha ACT Wazalendo kizingatie masharti ya kanuni ya 35 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025 inayohusu utaratibu na ratiba za kampeni za ubunge.

Send this to a friend