Tumepiga hatua katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji nchini lakini bado tunayo kazi kubwa ya kufanya

0
39

Amaniel Ngowi, Chuo Kikuu

Mwaka wa 2020 unaelekea ukingoni na ni kawaida yetu binadamu kufanya tafakari ya nini tumefanya kwa mwaka tunaomalizia na kuweka malengo ya mwaka ujao wa 2021.

Hatua kubwa katika uchumi wa Tanzania kwa mwaka huu wa 2020 ni ile ya kuingia katika kundi la nchi za uchumi wa kati, ikiwa ni miaka mitano kabla ya muda ambao nchi ilikuwa imejiwekea. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia ambayo ndiyo hutoa orodha na hali ya afya ya uchumi wa nchi mbalimbali kila mwezi Julai, Tanzania ni moja ya nchi saba tu duniani ambazo ziliingia katika kundi hilo la uchumi wa kati kwa mwaka huu. Wataalamu wa uchumi wameunga mkono hatua hii kama hatua muhimu katika maendeleo ya nchi yetu.

Tukitazama mbele katika mwaka ujao wa 2021, ni vyema kukumbuka kwamba kuingia katika kundi la uchumi wa kati ni sehemu moja tu ya malengo mapana ya kukuza nchi yetu kiuchumi. Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025 ni pana zaidi. Kwamba kufika 2025 maendeleo yetu yawe yana kiwango cha juu zaidi cha maisha kwa wananchi, jamii iliyo na elimu bora na uchumi bora na ukuaji wa uchumi ulio endelevu.

Ili tuendelee kukuza uchumi wetu kwa kasi ambayo tumekuwa nayo hadi kufikia hatua hii muhimu, na ni lazima kuendelea kujenga mazingira bora ya uwekezaji kwa nguvu zetu zote.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Tanzania imeendelea kuwa sehemu nzuri ya kufanya biashara. Katika kipindi cha miaka mitano Urahisi wa Kufanya Biashara Tanzania umeongezeka toka asilimia 49.7 hadi asilimia 54.5 mwaka huu wa 2020.

Licha ya maendeleo haya, kama nchi tusibweteke.

Kuna mengi ya kuendelea kufanya ili kujenga mazingira bora zaidi ya kufanya biashara na uchumi imara. Mojawapo ya mambo ambayo lazima kuendelea kufanya ni kuhakikisha tuna sera bora zinazovutia kampuni mpya kuingia kuwekeza nchini.

Serikali imepiga hatua kubwa katika eneo hili. Mfano, pichani ni Rais Dkt John Magufuli alipozungumza na wafanyabiashara kuelewa kero zao na majawabu yake mwezi Juni mwaka jana. Serikali pia imejitahidi kupambana na mambo kama rushwa na vikwazo vya kuanzisha biashara.

Sehemu nyingine muhimu katika kujenga mazingira ya kuvutia uwekezaji ni kuweka mazingira bora ya mtu kuweza kutoka kwenye soko. Mfanyabiashara yeyote anapenda mazingira ya biashara ambayo ni rahisi kuingia na rahisi kutoka, mazingira ya kutojisikia kubanwa baada ya kuingia. Kuwa huru kuwekeza kadiri faida inavyomsukuma.

Kuendelea kujenga mazingira bora ya uwekezaji kutatusukuma kwenda mbali zaidi, kukuza uchumi wetu, ajira na heshima katika ulimwengu. Tumefanya vizuri 2020, tufanye vizuri zaidi 2021.

Send this to a friend