Tundu Lissu apingwa kwa madai ya kauli yake ya kibaguzi

0
42

Baada ya kauli iliyotafsiriwa kuwa ya kibaguzi iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu kukosoa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhusisha eneo analotoka, wananchi na viongozi mbalimbali wamemkosoa wakitaka kauli za kibaguzi kupingwa vikali.

Lissu alitoa kauli hiyo wakati akihutubia wananchi wa Babati mkoani Manyara ambapo alikosoa uamuzi wa kuwahamisha wananchi wa Ngorongoro na mambo mengine, akisisitiza kwamba “Rais kutoka Zanzibar hana mamlaka ya kutoa ardhi katika eneo hilo.”

Miongoni mwa walioonekana kuchukizwa na kauli hiyo ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, ambaye ameonya kwamba kauli hiyo ya kibaguzi inapaswa kulaaniwa, kwani inaweza kuathiri sana Muungano wa Tanzania.

“Hili tukilinyamazia litaota mzizi litabomoa taifa letu. Hatuwezi kukubali mtu mmoja kalewa na akaleweshwa na utu, ubinadamu na uungwana wa huyu wanayemuita Mzanzibar […] Nilitegemea chama chake na viongozi wake watamkemea, kwakuwa wameshindwa kumkemea, nataka kuliambia bunge hili, tuwaambie Watanzania wakikemee chama hiki na viongozi wao na tukitenge,” amesema.

Kwa upande wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Amos Makalla, ametoa msimamo wake akisisitiza kwamba Rais Samia Suluhu ni Rais wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, bila kujali eneo analotoka.

Mbunge ataka Serikali irejeshe utaratibu wa pasipoti kuingia Zanzibar

“Kauli hizi za hila, upotoshaji hazisaidii sana kujenga taifa letu. Ni kauli ambazo hazipaswi kuupuzwa wala kukaliwa kimya, na Watanzania wajue tunaye Rais mmoja, Samia Suluhu Hassan. Uhuru wa kufanya maandamano tuutumie vizuri lakini tutangulize Tanzania yetu,” ameeleza.

Aidha, kauli hiyo imekuwa na maoni tofauti kwa watumiaji wa mtandao wa X (zamani Twitter), baadhi ya wananchi na wanaharakati mbalimbali wameonekana kuchukizwa na kauli hiyo, wengine wakisema kuwa kauli hiyo inalenga kuwagawanya.

“Kuna tofauti kubwa baina siasa za hoja na siasa za ubaguzi! Tundu hizi ni siasa za UBAGUZI. Ni opportunism na siasi hizi zinaleta manufaa za mapito tu! Swali: Kwani sera ya CDM [CHADEMA] ni kutokuwa na Rais wa Tanzania kutoka ZNZ [Zanzibar] milele?” Fatma Karume ameandika katika mtandao wa X

Mwingine ni Lubasha Jr ambaye ameandika “Nadhani its fair kumkemea Samia anapokosea kama Rais wetu na sio Uzanzibar wake. Mwalimu [Julius Nyerere] aliwahi kusema dhambi ya ubaguzi huwa haina mwisho, tukianza kubaguana kwa Uzenji na Utanganyika, tutabaguana kwa makabila, na dini zetu, japo tunajua tuna wenzetu haya mambo wanafurahia sana.”

Aidha, kwa upande wake Khalifa Said ameandika “ni muhimu sana kwa wanasiasa kuchunga matamshi yao ili wasisaidie kuwagawa wananchi kulingana na maeneo wanayotoka na kujenga chuki baina yao. lissu angeweza kujenga hoja yake bila kushambulia u-zanzibari wa samia. hapa lissu amepotoka, ameruhusu hisia kutawala ubongo wake.”

Send this to a friend