TUNZAA yatangaza ushirikiano mkubwa na Vodacom kupitia M-PESA

0
55

Wateja wa Vodacom kuanza kutumia huduma za Tunzaa ndani ya aplikesheni ya M-Pesa Super App

Tunzaa Digital Holdings Limited (Tanzania), kampuni ya Kitanzania ya teknolojia ambayo imejikita katika kutatua changamoto za tabia za kifedha kwa Waafrika wa kila siku kwa kutumia teknolojia kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania PLC wamezindua rasmi ushirikiano utakaowawezesha wateja wa Tunzaa kutumia huduma zao kupitia aplikesheni ya M-Pesa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Muanzilishi wa Tunzaa Bwana Ng’winula Kingamkono alibainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019, Tunzaa imehudumia watumiaji zaidi ya 25,000 ambao wamejisajili kwenye jukwaa hilo, na imewezesha mamia ya wafanyabiashara wanaouza bidhaa zao mbalimbali kupitia Jukwaa la Tunzaa.

“Watumiaji wa Tunzaa wanawezeshwa kulipia bidhaa kidogo kidogo yaani ‘Hifadhi Sasa, Nunua baadae’ kwa kudunduliza kwa kipindi cha hadi miezi sita kwa bidhaaa yoyote atakayoichagua vikiwemo vifaa vya nyumbani, runinga, mashine za kufulia, majokofu, simu za mkononi, na vifaa vingine vingi. Lengo la Tunzaa ni kuimarisha tabia chanya za kifedha kwa Waafrika wa kila siku kwa kuwawezesha kununua bidhaa kwa njia ya awamu bila madeni,” alisema Bw. Ng’winula.

Kwa sasa Tunzaa inatoa huduma zake Tanzania nzima na hapo baadae ina lengo la kutanua wigo kufikia nchi za jirani kama Kenya, Uganda, Kongo, Zambia, Malawi, Msumbiji na baadae kufikia nchi zote za Kiafrika. Huduma hii inapatikana kwa kupakua aplikesheni ya Tunzaa kupitia simu janja, aidha Android ama iOS, pia watumiaji wanaweza kununua bidhaa kwa kutembelea tovuti ya Tunzaa yaani www.tunzaa.co.tz

“Tunzaa ina furaha kutangaza ushirikiano wa kipekee na kampuni ya Vodacom Tanzania kupitia aplikesheni ya M-Pesa.ambapo kuanzia leo wateja wote wa Vodacom wanaotumia huduma ya M-Pesa kwa ajili ya kufanya miamala yao wataweza kupata huduma ya kununua bidhaa mbalimbali kwa kulipa kidogo kidogo kutoka kwenye aplikesheni ya Tunzaa inayopatikana ndani ya aplikesheni ya M-Pesa moja kwa moja. Huduma zote za Tunzaa sasa zitafanyika ndani ya aplikesheni ya M-Pesa, hatua hii itasaidia watumiaji wa M-Pesa kuweza kufanya miamala na kununua bidhaa wakiwa wanaendelea na huduma nyingine za M-Pesa,” alimalizia Muanzilishi huyo.

Ushirikiano huu unaashiria hatua kubwa katika biashara za kimtandao kwani Tunzaa kwa kushirikiana na M-Pesa wanatoa suluhisho rahisi la manunuzi ya kimtandao na kuongeza uhuru wa kifedha kwa Watanzania na Waafrika kwa ujumla na lengo la jukwaa hili ni kuwawezesha Waafrika wa kawaida kwa kupata njia salama, bora, na endelevu ya kupata bidhaa na huduma wanazohitaji.

Kwa upande wa Vodacom, Bi. Josephine Mushi ambaye ni Meneja wa Chaneli za Kidijitali na Malipo kwa Mtandao alisema “Tuna furaha kubwa kuwakaribisha Tunzaa kwenye familia ya M-Pesa ambayo ina watoa huduma takribani ishirini na bado tunaendelea kukua. Kupitia ushirikiano huu, wateja wetu wataweza kufikia jukwaa la “Hifadhi Sasa Nunua Baadaye” la Tunzaa moja kwa moja ndani ya programu ya M-Pesa, bila haja ya kutumia programu tofauti. Azma yetu ni kuchochea mtindo wa maisha wa kidigitali na haswa malipo ya kidigitali kwani yanahakikisha usalama wa miamala na vile vile huwezesha watumiaji kuwa na rekodi ya matumizi yao.”

Kwa miaka kumi na tano sasa, M-Pesa imekua ikichochea ujumuishi wa kifedha rasmi na inaaminiwa na Watanzania zaidi ya milioni 17. Kwa sababu hiyo na nyingine nyingi, Tunzaa na M-Pesa wanaamini kwamba ushirikiano huu utakuwa na faida kubwa kwa kufungua njia mpya za upatikanaji wa bidhaa na hivyo kupelekea uhuru wa kifedha kuongezeka maradufu. Hii itachochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali sambamba na malengo ya serikali.

Kwa habari zaidi kuhusu Tunzaa na ushirikiano wake na M-Pesa, tafadhali tembelea tovuti ya Tunzaa www.tunzaa.co.tz au kurasa za Tunzaa katika mitandao ya kijamii.

Kuhusu Tunzaa

Tunzaa ni jukwaa la kipekee la “Hifadhi Sasa Nunua Baadaye” lililobuniwa kwa lengo la kuwawezesha Waafrika wa kawaida kupata njia ya kununua bidhaa kwa awamu bila deni. Kwa dhamira ya kuingiza kifedha, Tunzaa inatoa njia salama, bora, na endelevu kwa watumiaji kupata bidhaa na huduma wanazohitaji.

Send this to a friend