
Mwigizaji na mwandishi wa filamu, Derek Dixon, amemshtaki Tyler Perry kwa madai ya unyanyasaji wa kijinsia katika kesi iliyowasilishwa wiki iliyopita katika Mahakama Kuu ya Los Angeles, Marekani.
Dixon anadai kuwa Perry alimsumbua kwa mara kadhaa kwa kumtaka kimapenzi bila ridhaa yake, na alijaribu kuficha jambo hilo kwa kumwahidi kumuendeleza kwenye kazi ya kuandika kipindi.
Dixon anasema tukio la kwanza lilitokea mwaka 2019 nyumbani kwa Perry mjini Georgia, baada ya kufahamiana kwenye hafla ya uzinduzi wa studio zake. Baadaye alipewa nafasi ndogo kwenye kipindi cha ‘Ruthless’ na kisha akapata nafasi kubwa zaidi kwenye kipindi ‘The Oval’.
Katika kesi hiyo, Dixon anadai kuwa Perry alikuwa akimpigia simu na kumtumia jumbe mara kwa mara, akimtaka kimapenzi na kisha kumtaka kimwili mara mbili; kwenye sherehe ya waigizaji Bahamas mwaka 2020 na tena nyumbani kwa Perry mwaka 2021.
Mawakili wa Perry wamekanusha madai hayo, wakisema kuwa Dixon alijaribu kuwa karibu Perry ili amtapeli na madai hayo hayana msingi. Dixon anadai fidia ya dola milioni 260 [TZS bilioni 674] kwa kile anachokieleza kama mateso ya muda mrefu na kisasi kazini baada ya kukataa matakwa ya Perry.