UAE yaingia makubaliano na DR Congo katika uchimbaji wa madini

0
40

Ujumbe wa maafisa wa Umoja wa Falme za Kiarabu umesaini mkataba wa ushirikiano wenye thamani ya dola bilioni 1.9 [TZS trilioni 4.6] kwa ajili ya kuendeleza migodi kadhaa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mkataba huo umesainiwa na kampuni ya madini ya serikali inayojulikana kama Societe Aurifere du Kivu et du Maniema (Sakima), kulingana na taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais Felix Tshisekedi kupitia tovuti yake.

Ndege za ATCL hatarini kukamatwa

Ujumbe kutoka Falme za Kiarabu uliongozwa na waziri wa serikali katika wizara ya mambo ya nje, Shakhbut Nahyan Al Nahyan, na mkutano huo ulifanyika huko Kinshasa, mji mkuu wa Congo.

Ushirikiano huo “utawezesha kuanzishwa kwa migodi zaidi ya minne ya viwanda ambayo itaunganisha mikoa ya Kusini Kivu na Maniema,” imesema taarifa kutoka ofisi ya Rais ambayo haikutoa maelezo kuhusu migodi au madini yanayohusika.

Mikoa ya Kusini Kivu na Maniema ni tajiri kwa dhahabu, shaba, na tantalum. Mikoa hiyo imeathiriwa kwa miongo kadhaa na vurugu zinazosababishwa na makundi yenye silaha, ambayo mara nyingine hujipatia fedha kupitia biashara haramu ya madini.

Serikali ya Congo na kampuni ya Falme za Kiarabu, Primera Group Ltd., walishirikiana na kuanza kusafirisha dhahabu iliyochimbwa kwa njia za jadi kutoka Kusini Kivu mwanzoni mwa mwaka huu.

Send this to a friend