Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani umethibitisha kuwa Watanzania 24 wanashikiliwa na Mamlaka ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE) kwa kuishi nchini humo bila vibali halali.
Ubalozi umesema kati ya hao, wanne wamekamilisha taratibu zote za kisheria za kurejeshwa nchini na wanatarajia kurudishwa Tanzania wakati wowote na wengine 20 bado wanaendelea na kesi za uhamiaji nchini Marekani.
Ubalozi umeeleza kuwa haujapewa taarifa rasmi kuhusu tarehe maalum ya kurejeshwa kwa Watanzania hao, lakini tayari umeombwa kutoa hati za kusafiria kwa wawili kati ya wanne waliopangiwa kurejeshwa. Hii inaashiria kuwa mchakato wa kuwarejesha unaweza kufanyika wakati wowote.
Ripoti ya hivi karibuni ya ICE inaonyesha kuwa hadi Novemba 24, 2024, jumla ya wahamiaji haramu 1,445,549 kutoka mataifa mbalimbali waliorodheshwa kwa ajili ya kurejeshwa makwao. Miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki, Kenya ina idadi kubwa zaidi ya watu waliothiriwa (1,282), ikifuatiwa na Burundi (462), Uganda (393), Rwanda (338), na Tanzania (301).
Ubalozi umefafanua kuwa Watanzania watakaorejeshwa kutoka Marekani hawatakabiliwa na vikwazo vya kusafiri kwenda nchi nyingine. Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria za sasa za uhamiaji za Marekani, wataweza kuomba viza ya kurejea nchini humo baada ya miaka kumi.
Aidha, watakapowasili Tanzania, wahamiaji hao watapokelewa na Idara ya Uhamiaji, na baada ya kukamilisha taratibu zote za uhamiaji, watakuwa huru kuendelea na maisha yao kama raia wa Tanzania.
Mkurugenzi wa Ofisi ya Diaspora ya Tanzania, Kelvin Nyamori, amebainisha kuwa mchakato wa kurejesha wahamiaji utakuwa mgumu zaidi kwa wale waliotumia utaifa wa uongo kupata hadhi ya ukimbizi. Amesema baadhi ya watu hudanganya ili kupata nyaraka kutoka nchi nyingine, jambo ambalo linaweza kuleta changamoto katika mchakato wa kurejeshwa kwao.
“Kila nchi ina sheria zake za uhamiaji. Ikiwa uliondoka Tanzania, huwezi kusema uongo kuhusu vita au hadhi ya ukimbizi, kwani Tanzania haina migogoro ya aina hiyo. Baadhi ya watu hudanganya ili kupata nyaraka kutoka nchi nyingine,” amesema Nyamori.
Ubalozi umewakumbusha Watanzania kuwa kuishi katika nchi yoyote bila kuwa na nyaraka halali ni kosa kisheria.