Ubalozi wa Tanzania watoa tahadhari kwa wanunuaji wa malori Uingereza

0
111

Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza umetoa tahadhari kwa wafanyabiashara wenye nia ya kununua malori yaliyotumika kutoka Uingereza kuchukua tahadhari za msingi wanapofanya manunuzi hayo ili kuepuka usumbufu na hasara inayoweza kutokea.

Tahadhari hiyo iliyotolewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mbelwa Kairuki ni kufuatia ubalozi kupokea malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara ambao wametuma pesa nchini Uingereza kwa ajili ya kununua malori, lakini hawajatumiwa magari yao kwa muda unaozidi miezi sita, na wengine waliotumiwa wamepokea malori yaliyo chini ya kiwango na kupelekea hasara kubwa.

Kwa muktadha huo, Ubalozi umewataka wafanyabiashara wenye nia ya kununua malori nchini humo kufanya mambo matano muhimu ambayo ni; kufuatilia ikiwa kampuni wayotaka kufanya nayo biashara imesajiliwa nchini Uingereza (ipo active), ambapo uhakiki huo unaweza kufanywa kupitia tovuti ya Serikali ya Uingereza isiyo na malipo ya https://gov.uk/get-information-about-a-company….

Kuingia mkataba wa manunuzi na kampuni inayokuuzia lori, akifafanua kuwa wapo Watanzania wanadiaspora wenye Ofisi za sheria (law firms) nchini Uingereza ambao wanaweza kutoa huduma ya kuandaa mikataba, na inapojitokeza changamoto zozote ni rahisi kwa wao kufuatilia.

Kufanya malipo kwa kutumia Letter of Credit (LoC) [barua ya mkopo] badala ya kutuma pesa taslimu moja kwa moja kwa kampuni kwa njia ya Telegraphic Transfer (TT). Balozi Kairuki amesema utaratibu wa Malipo kwa LoC unasaidia kumlinda mfanyabiashara pale muuzaji anapokiuka makubaliano, na kwamba maelezo kuhusu kulipa kwa LoC yanapatikana katika benki zote nchini.

Kufanya upekuzi wa kufahamu historia ya lori unalotaka kununua kabla ya kufanya malipo. Ameeleza kuwa ili kufanikisha upekuzi huo, ni vyema upate namba za usajili wa gari za nchini Uingereza kisha elekea katika tovuti ya Serikali ya Uingereza ambayo ina mfumo wa kutoa taarifa ya historia nzima ya gari kama liliwahi kupata ajali, limefanyiwa ‘check up’mara ngapi nk. kupitia Tovuti : https://gov.uk/check-mot-history…

Kufanya ukaguzi kabla ya gari kusafirishwa (pre-shipment inspection) ili kujihakikishia kwamba kinachotumwa kinaendana na makubaliano kati yako na muuzaji.