Uber yasitisha baadhi ya huduma zake Tanzania
Uber Tanzania imetangaza kusitisha huduma zake za UberX, UberXL na UberX Saver nchini Tanzania kuanzia leo Aprili 14, 2022.
Katika taarifa yake kampuni hiyo imesema kuwa kanuni za sasa za usimamizi wa sekta hiyo si rafiki na zimekuwa changamoto kubwa katika uendeshaji wa biashara ya usafiri, na hivyo wanasitisha hadi hape muafaka utakapopatikana.
“Huu ni wakati mgumu kwetu sote, lakini haina maana kwamba ndio mwisho wa kila kitu,” imeeleza kampuni hiyo ikiongeza kuwa “tuko tayari kushirikiana na mamlaka husika na kuwa na mazungumzo yatakayoleta tija.”
Taarifa ya Uber kusitisha huduma zake ni mwendelezo wa changamoto katika sekta ya usafiri ambapo kutokana kupanda kwa bei za mafuta wafanyabiashara wa usafiri wamekuwa wakiishinikiza serikali kupitia upya nauli za mabasi ya mijini na safari ndefu.