Kampuni ya Dhahabu ya Barrick imeingiza zaidi ya shilingi trilioni 10.1 katika uchumi wa Tanzania tangu kuanzishwa kwa ubia wa Twiga kati yake na Serikali ya Tanzania mwaka 2019, na kuchangia shilingi trilioni 2 mwaka 2024 pekee.
Katika mkutano na waandishi wa Habari, Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, amesema ubia wa Twiga unaohusisha migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu umeendelea kufanya vizuri katika sekta ya uchimbaji madini nchini Tanzania, ukichangia maelfu ya ajira, kusaidia biashara za ndani na kufadhili miradi muhimu ya kijamii.
Ameongeza kuwa kutokana na sera ya Barrick ya kuendeleza ajira na maendeleo ya ndani,asilimia 96 ya wafanyakazi wa Barrick nchini Tanzania, wapatao 6,185, ni Watanzania, huku asilimia 53 wakitoka katika jamii zinazozunguka migodi.
Migodi ya Bulyanhulu na North Mara ilifanya vizuri katika utekelezaji wa uzalishaji wa mwaka 2024, ikiendelea kuzingatia usalama wa hali ya juu, na kutimiza mwaka mzima bila matukio yoyote ya majeraha makubwa yaliyoweza kupunguza muda wa kazi.
“Tulitumia dola milioni 573 kwa wasambazaji na watoa huduma wa ndani mwaka jana, sawa na asilimia 83 ya matumizi yetu yote. Aidha, asilimia 75 ya malipo yetu yote kwa watoa huduma na wasambazaji yalikwenda kwa makampuni ya wazawa, yakivuka lengo letu la asilimia 61,” amesema Bristow.
Ameongeza, “Mnamo mwaka huo huo, Barrick iliwekeza zaidi ya dola milioni 5 katika miradi ya maji safi ya kunywa, huduma za afya, na elimu, na kufanya jumla ya uwekezaji katika miradi ya kijamii kufikia dola milioni 15.8 tangu Barrick ichukue jukumu la uendeshaji wa migodi ya Tanzania mwaka 2019.”
Kwa upande wa mgodi wa Buzwagi, ameeleza kuwa mgodi huo ulifanya maendeleo makubwa katika utekelezaji wa ufungwaji wake, huku ukizingatia usimamizi wa mazingira, hasa kuhusu maji na utunzaji wa uoto wa mimea.