Uchaguzi Mkuu Tanzania 2020: Wasifu wa Dkt. Hussein Mwinyi

0
50

Na Farid Hashim, Zanzibar

Juni 12 mwaka huu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole aliitangaza Juni 15 kuwa siku ambayo zoezi la kuchukua fomu kwa watia nia wa nafasi ya Urais Bara na Zanzibar litaanza. Siku 5 baadaye, yani Juni 17 Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt Hussein Ali Mwinyi alijitokeza katika Ofisi za CCM zilizopo Kisiwandui Mjini Unguja, na kuchukua fomu hizo. 

Baada ya kukamilisha zoezi hilo, baadhi ya wanahabari walimtaka Dkt Mwinyi kuzungumza lakini hata hivyo aliwaomba radhi kwamba asingeweza kwa wakati huo. Mwinyi alieleza kwamba angependa kwanza kwenda kutulia na kusoma vizuri fomu hizo na kutekeleza yanayohitajika, na kisha katika wakati muafaka angezungumza na waandishi wa habari na wananchi. 

Dkt Mwinyi ni mmoja ya makada mashuhuri wa CCM ambao wametajwa kwa miaka mingi kuweza kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar pale Rais wa sasa Dkt Ali Mohamed Shein atakapomaliza muda wake. 

Zoezi la kuchukua fomu hizo bado linaendelea, na makada mbalimbali bado wanaendelea kujitokeza. Katika mfululizo wa makala za Swahili Times kutazama wasifu wa makada mbalimbali, makala hii inatazama wasifu mfupi wa Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Dkt Mwinyi alizaliwa kisiwani Unguja Ijumaa Disemba 23 mwaka 1966. Kitaaluma Mwinyi ni daktari wa binadamu, ambapo Shahada yake ya Udaktari (MD) alitunukiwa mwaka 1992 katika Chuo Kikuu cha Marmara kilichopo jijini Istanbul nchini Uturuki. Baada ya kupata shahada yake alikwenda kujiongeza ujuzi nchini Uingereza, na mwaka 1993 akapata Stashahada ya Juu (Postgraduate Diploma) katika eneo tiba la Internal Medicine kutoka Shule ya Tiba ya Hospitali mashuhuri ya Hammersmith (The Royal Postgraduate Medical School, Hammersmith Hospital). Mbali na kujiongeza ujuzi, Mwinyi alitumia digrii yake ya kwanza ya tiba toka Uturuki na Stashahada hiyo ya Juu toka Uingereza kuanza masomo yake ya digrii ya pili katika tiba hapo hapo Hammersmith Uingereza, ambapo alihitimu mwaka 1997. Kuhitimu huko kulimtunuku pia Uanachama wa Kudumu katika Familia ya Madaktari ya Uingereza(Membership of the Royal College of Physicians — MRCP). Mwinyi pia ni mwanachama wa Chama cha Matabibu Tanzania. 

Mwinyi aliingia katika ajira tangu akiwa mwanafunzi. Mwaka 1992 hadi 1993 alikuwa Afisa Nyumba(House Officer) kwenye Kitengo cha Utabibu wa Figo (Nephrology Unit) cha Hospitali ya Kifalme ya Sussex huko Brighton nchini Uingereza. Mwaka 1994 hadi 1995 akafanya kazi kama Afisa wa Juu wa Nyumba kwenye Shule ya Tiba ya Hospitali ya Hammersmith jijini London nchini Uingereza. 

Mwaka 1996 hadi 1997 akawa nchini Tanzania akifanya kazi kama Msajili (Registrar) kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam. Baada ya Muhimbili, kwa muda wa miaka miwili kati ya mwaka 1998 hadi 2000 akajiunga na Hospitali ya Kumbukumbu ya Hubert Kairuki jijini Dar es Salaam kama Daktari Bingwa na Mhadhiri Mwandamizi kwenye Chuo cha Tiba Hubert Kariuki. 

Hussein Mwinyi aliingia katika utumishi wa umma kwenye siasa mwaka 2000 baada ya kuchuana katika kura za maoni ndani ya CCM na kufanikiwa kugombea Ubunge Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani ambako alishinda kiti hicho. 

Baada ya kushinda kiti cha Ubunge, Mwinyi pia aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania. Januari 2006 hadi Februari 2008 Mwinyi alihudumu kama Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais akishughulikia Mambo ya Muungano. Mwezi Februari mwaka huo wa 2008 akateuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa nafasi ambayo alidumu mpaka Mei 2012. 

Baada ya kumaliza kipindi chake cha kwanza cha Ubunge Mkuranga, Mwinyi aliamua kugombea Ubunge katika Jimbo la Kwahani Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005 kwa tiketi ya CCM na kufanikiwa kushinda kiti hicho ambacho amehudumu kwa miaka 15 sasa. 

Tukiendelea na wasifu wake katika Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mei 2012 Mwinyi akateuliwa kuwa Waziri wa Afya akitokea Uwaziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Alihudumu katika nafasi hiyo ya Waziri wa Afya hadi Januari mwaka 2014. Mwezi huo huo wa Januari 2014 aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na kuhudumu hadi Novemba 2015. Disemba 2015 akateuliwa tena kuwa Waziri wa wizara hiyo hiyo ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, nafasi ambayo anahudumu mpaka sasa. 

Katika Kamati za Bunge la Tanzania, kwa miaka 12 (toka Februari 2008 hadi Bunge lilipovunjwa mwezi huu) Mwinyi amekuwa Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Masuala ya Usalama. 

Zaidi ya makada 10 wa CCM tayari wamechukua fomu kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea Urais Zanzibar. Mbali na Dkt Mwinyi,makada wengine ni Jecha Salum Jecha, Balozi Ali Karume, Mbwana Juma, Profesa Makame Mbarawa, Shamsi Nahodha, Omari Musa, Meja Jenerali mstaafu Suleiman Nassor, Mohamed Hija, Mohamed Jumanne, Mwantum Mussa Sultan (mwanamke pekee mpaka sasa) na Mbwana Yahya. Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wanatarajiwa kufanya uteuzi wa kada mmoja kwenye nafasi hiyo siku ya Jumapili Julai 12 2020. 

Send this to a friend