Uchaguzi Mkuu Tanzania 2020: Wasifu wa Profesa Makame Mbarawa

0
60

Na Wahida Omari, Zanzibar

Waziri wa Maji na kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),  Profesa Makame Mbarawa amechukua fomu kuomba ridhaa ya chama chake kuwania Urais wa Zanzibar 2020. Tukio hilo limefanyika leo Juni 19 majira ya saa nne asubuhi katika Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui, ambako Profesa Mbarawa amekabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa Oganaizesheni wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Galous Nyimbo.

Prof. Makame Mnyaa Mbarawa alizaliwa mwaka 1961 katika kisiwa cha Pemba na kupata elimu  ya  msingi na sekondari  katika Skuli ya Chokocho  iliyopo  Wilaya ya Mkoani. Baada ya hapo alipata elimu ya  ufundi katika Chuo cha Ufundi cha Karume Mbweni, Zanzibar na kuhitimu mwaka 1981 na kisha kuanzia mwaka 1982 hadi 1985 alifanya kazi katika Idara ya Usafiri Baharini, Wizara ya Mawaswiliano na Uchukuzi, Zanzaibar pamoja na Shirika la Meli Zanzibar. 

Mwaka 1985 alifadhiliwa na serikali ya Tanzania kwenda kusoma nchini Urusi katika fani ya Uhandisi wa Mitambo ya meli (Marine Engineering) kwenye Chuo cha  Astrakhan Technical Institute of Fisheries ambako alihitimu Shahada ya Uzamili (Masters) katika fani ya uhandisi Mitambo ya Meli mwaka 1992. Baada ya kuhitimu alirudi Zanzibar na kuendelea na kazi katika Shirika la Meli la Zanzibar hadi mwaka 1994. 

Mwaka 1994 Mbarawa alirudi tena darasani hadi mwaka 1999 aliphitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha New South Wales, Sydney – Australia katika fani ya Uhandisi Mitambo (Mechanical Engineering).

Mwaka 1999, alikuwa Mkufunzi katika Chuo Kukuu cha Stallenbosch, Afrika Kusini na Mtafiti chuoni hapo katika Kituo cha Uhandisi wa Magari. Mwaka 2000, alifanya kazi katika Chuo cha Technikon Pretoria kama Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Uhandisi Mitambo kabla ya kupanda na kuwa Proesa Mshiriki chuoni hapo mwaka kisha Profesa Kamili mwaka 2009. 

Ndani ya Chama Cha Mapinduzi CCM, Profesa Mbarawa alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuanzia mwaka 2007 hadi 2017, na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi kuanzia mwaka 2012 hadi 2017.

Profesa Mbarawa aliteuliwa kuwa Mbunge na kisha Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kuanzia mwaka 2010 hadi 2015. Kuanzia mwaka 2015 hadi 2018 Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli alimteua Profesa Mbarawa kuwa Mbunge na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Mwaka 2018  Rais Magufuli alimteua Profesa Mbarawa kuwa Waziri wa Maji. 
Mpaka sasa, Profesa Mbarawa anakuwa kada wa 10 wa CCM kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea Urais wa Zanzibar. Makada wengine ni Balozi Ali Karume, Mbwana Juma, Shamsi Nahodha, Omari Musa, Meja Jenerali mstaafu Suleiman Nassor, Mohamed Hija, Dkt Hussein Mwinyi, Mohamed Jumanne na Mbwana Yahya. Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wanatarajiwa kufanya uteuzi wa kada mmoja kwenye nafasi hiyo Julai 12 2020.

Send this to a friend