Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni amesema kuwa uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi kuhusu basi lililosababisha ajali wiki mbili zilizopita na kusababisha vifo vya watu 22 mkoani Morogoro, umeonesha kuwa lilitengenezwa kwa kutumia vifaa vya ujenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo wakati akitoa taarifa ya utafiti wa vyanzo vya ajali uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema uchunguzi umebainisha kuwa baadhi ya vifaa vilivyofungwa kama ‘ringboard’ hutumika kuweka zege kwenye ujenzi wa nyumba.
“Hizi ni Ringboard ambazo hutumika kuweka zege katika nyumba ndizo zimewekwa kwenye ‘chesis’ ya gari, na hizi ndizo zimekata viungo vya Watanzania,” amesema Masauni.
Waziri Masauni ameagiza kufanyika msako nchi nzima kwa magari yote yaliyofanyiwa hivyo, pia kumsaka mara moja mmiliki wa gari hilo pamoja na kiwanda kilichofunga kifaa hicho ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Hata hivyo utafiti wa UDSM umebaini kuwa vyanzo vya ajali vinatokana na mambo makuu matatu, yakiwa ni uzembe wa madereva, uchakavu wa magari na miundombinu ya barabara.
Kwa mujibu wa tafiti, uzembe wa madereva unachangia ajali kwa asilimia 76, huku ubovu wa mabasi asilimia 18, na miundombinu ya barabara asilimia 6.
Kutokana na utafiti huo, Waziri Masauni ameagiza Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani kuanzia leo Machi 31, 2022, mabasi yote na malori yawe na vidhibiti mwendo kwa sababu baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri wamekuwa wakivitoa vidhibiti hivyo.