Uchunguzi kufanyika mjamzito aliyefariki kwa kukosa fedha za kuweka mafuta gari la wagonjwa

0
79

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka ametoa siku tatu vyombo vya usalama kuchunguza tukio la mama mjamzito aliyefariki baada ya familia yake kukosa pesa za kuweka mafuta gari la wagonjwa.

Shaka alipokea tuhuma hizo kutoka kwa mume wa marehemu, Seleman Makuani wakati akisikiliza kero za wananchi katika Kata na Kijiji cha Kidodi, mkoani humo.

Akisimulia tukio hilo, amesema mke wake aliyejulikana kwa jina la Zaituni Mayuga alichelewa kupatiwa huduma za matibabu wakati akitaka kujifungua kwa kulazimishwa kulipia gharama za mafuta TZS 180,000 kwa ajili ya kuweka mafuta.

Ameeleza kuwa ilimchukua muda mrefu mke wake kusafirishwa kutoka Kituo cha Afya Kidodi kwenda Hospitali ya Mtakatifu Kizito Mikumi kutokana na kukosa fedha hizo hadi pale alipotoa kiasi cha TZS laki 1, ikiwa ni muda mrefu umepita jambo ambalo lilisababisha kupoteza maisha.

Akizungumza Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kidodi, Elia Mwakibete amesema gari hilo la wagonjwa halikuwa na mafuta nahata dereva bado hajaletwa.