Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema uchunguzi umebaini baadhi ya watuhumiwa kupata madhara ya mwili na wakati mwingine kupoteza maisha kutokana na kupigwa na kuteswa wakati wa ukamataji ama wakati wa upelelezi.
Akizungumza hayo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na tathmini hiyo, Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu amebainisha namna hiyo ya upataji wa taarifa za uhalifu zinazofanywa na Jeshi la Polisi.
“Tathmini ya jumla kwa nyakati tofauti kumekuwa na malalamiko kutoka kwa watuhumiwa na wananchi, na wakati mwingine kupitia vyombo vya habari kulalamikia Jeshi la polisi kuhusu matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora,” amesema Jaji Mwaimu.
Aidha amesema mwaka 2020 hadi 2022 wamekuwa wakifuatilia mwenendo na utendaji kazi wa Jeshi la polisi kwa kufanyia uchunguzi matukio kadhaa kuhusu tuhuma dhidi ya Jeshi hilo na kutembelea vituo vya polisi katika baadhi ya mikoa ya Tanzania.
Ameongeza kuwa THBUB imebaini askari polisi wanaopatikana na hatia hupewa adhabu isiyowiana na makosa yao, na kuongeza kuwa makosa yanayofanywa na askari polisi yenye mwelekeo wa kijinai yachunguzwe kwanza na taasisi nyingine huru za umma ama vyombo vitakavyoundwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, amesema kwa ajili ya kuongeza ufanisi, Jeshi la Polisi litekeleze mapendekezo yaliyotolewa na tume, na kuitaka Serikali kulipatia vitendea kazi, kuendelea kuwajengea makazi bora, kuimarisha miundombinu na kuongeza idadi ya askari.