Uchunguzi umedai wanafunzi walijichora tattoo kwa mapenzi yao

0
79

Baada ya taarifa kusambaa mitandaoni kuhusu wanafunzi kuchorwa ‘tattoo’ na mwanafunzi mwenzao anayedaiwa kutumwa na dada wa kazi, na wengine kuzihusisha na imani za kishirikina, uchunguzi umebaini kuwa wanafunzi hao walijichora kwa mapenzi yao.

Akizungumza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa kipolisi Kinondoni, Khamis Kingai amesema baada ya kupata taarifa hiyo waliifuatilia na kugundua hakuna kosa la kijinai ambalo wanaweza kulipelekeza ila zaidi ni suala la kinidhamu.

“Kijinai hatuoni kama kuna kosa la mtu kujichora tattoo kwenye mwili wake. Amejichora mwenyewe, halafu siyo kama amelazimishwa, siyo kama amejeruhiwa kwa kuchomwa moto, ametaka mwenyewe,” amesema.

Aidha, Ofisa Elimu Msingi Manispaa ya Kinondoni, Theresia Kyaria amesema hatua nyingi zilichukuliwa kupitia polisi, dawati la kijinsia na kubaini kuwa msichana wa kazi wa nyumbani kwa mwanafunzi huyo amejichora tattoo, na ndipo  mtoto huyo alipomuona alivutiwa na kwenda kuchora shuleni na wenzake wakamuiga.

“Tulibaini baadhi wana vidonda ndipo wakapelekwa kituo cha afya kwa matibabu kwanza ili vidonda vipone na pili kuangalia kama kuna athari zozote za kiafya wamepata, tumebaini hakuna athari zozote za kiafya, wachache waliokuwa na vidonda vilitibiwa na wameshapona,” amesema.

Amesema Juni 6 walikaa kikao na wazazi takribani 600 na wamekubaliana mambo mbalimbali ikiwemo namna ya kuwasaidia watoto waondokane na matendo yasiyofaa katika jamii.

Send this to a friend