Ufafanuzi wa Polisi kuhusu kifo cha mgombea Uenyekiti kupitia CHADEMA

0
17

Jeshi la Polisi limefafanua juu ya kifo cha Joseph Remigius (52) mkazi wa Kijiji cha Karagara, Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera ambaye alikuwa ametia nia ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), likieleza kuwa chanzo cha kifo chake kinatokana na ajali na si kama inavyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime imeweka wazi kuwa Oktoba 31, 2024 majira ya saa tatu usiku, Remigius alitoka bar waliyokuwa wanakunywa pombe akiwa amebebwa kwenye bodaboda na kupata ajali, na baada ya ajali hiyo walipata msaada na kufikishwa katika Kituo cha Afya Minziro ambapo walipatiwa matibabu na kuruhusiwa.

DCP Misime ameongeza kuwa Novemba 1, 2024 majira ya saa kumi alfajiri, taarifa zilipokelewa katika Kituo Kidogo cha Polisi Minziro kuwa Joseph Remigius amefariki dunia akiwa nyumbani kwake.

“Hadi sasa kulingana na ushahidi wa mashuhuda wa ajali na waliompatia msaada na kumfikisha katika Kituo cha Afya Minziro, ajali ndiyo chanzo cha kifo chake,” imeeleza taarifa ya Jeshi la Polisi.

Aidha, DCP Misime ametoa wito kwa wananchi kuwa endapo kuna mwenye ushahidi tofauti na huo wa mashuhuda wa ajali basi aufikishe Polisi ili ufanyiwe kazi.

Send this to a friend