Ufafanuzi wa Polisi kuhusu madai ya Kigwangalla kumpiga risasi mlinzi

0
38

Kufuatia taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimhusisha mbunge wa jimbo la Nzega Vijijini na mmiliki wa kiwanda cha kuchakata pamba kiitwacho Mwalujo Ginery, Hamisi Kigwangalla kudaiwa kumpiga risasi mlinzi wake, Jumanne Misango (66), Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limesema uchunguzi umebaini hakuna jeraha wala mvunjiko wowote wa mifupa katika mwili wa mlinzi huyo.

Jeshi la Polisi limesema taarifa za awali zinaonesha kuwa kulitokea wizi wa mali mbalimbali zenye thamani ya TZS milioni 28.5 kiwandani hapo kilichopo Kijiji cha Mwalujo, Wilaya ya Kwimba mkoani humo ambapo Kigwangalla alifika kiwandani na kutokea majibizano kati yake na mlinzi wake, ndipo mlinzi huyo alitoa taarifa polisi kuwa ameshambuliwa na kupigwa risasi katika mguu wake wa kulia.

Orodha ya majina ya vijana wote waliochaguliwa kwenda JKT na kambi zao

“Baada ya taarifa hiyo kupokelewa, askari walifika eneo la tukio na kufanya ukaguzi ambapo hakukuonekana viashiria vyovyote vya matumizi ya silaha ya moto. Hata hivyo Jumanne alipewa PF3 na kwenda hospitali ya Wilaya ya Kwimba kwa uchunguzi wa kitabibu, Kigwangalla alihojiwa na kufunguliwa kesi ya shambulio, na yuko nje kwa dhamana,” imeeleza taarifa ya polisi.”

Aidha, Jeshi la Polisi limesema Misango amefunguliwa jalada la uchunguzi kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwa Afisa wa Polisi na kuzua taharuki kwa jamii kuwa amepigwa risasi.

“Upelelezi wa kesi hizo mbili unaendelea na utakapokamilika watuhumiwa wote wawili watafikishwa mahakamani,” imeeleza.

Send this to a friend