Ufafanuzi wa TEMESA kuhusu gharama za matengenezo ya MV Magogoni

0
49

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imesema gharama za sasa za ujenzi wa kivuko kipya cha MV. Magogoni zinaweza kuwa zaidi ya mara nne ya gharama za kivuko hicho kwa mwaka 2008 wakati kilipotengenezwa.

Akizungumza na Swahili Times wakati akifafanua taarifa za ukarabati wa kivuko hicho ambacho gharama zake ni TZS bilioni 7.5, Meneja Vivuko Kanda ya Mashariki, Lukombe King’ombe amesema gharama hizo ni kutokana soko ambalo hutegemea na hali ya kidunia inavyokwenda.

“Gharama za [mwaka] 2008 zinazozungumziwa (TZS bilioni 8.5) haziwezi kuwa sawa na 2023, gharama za ujenzi wa vivuko zinategemeana na soko. Kuna vitu vingi vinavyoendelea duniani ikiwemo vita ya Ukraine, wakati kinajengwa 2008 hivyo vitu havikuwepo. Hata tukitangaza tenda hiyo leo huwezi kujenga kivuko kipya chenye ukubwa wa MV. Magogoni kwa gharama hiyo,” ameeleza.

Amefafanua kuwa “kivuko cha Magogoni kinaweza kubeba abiria 2,000 na magari 60 madogo. Mara ya mwisho tumejenga kivuko cha MV. Kazi mwaka 2016 kwa bilioni 7.8 na kinaweza kubeba abiria 800 na magari 22, Magogoni ni zaidi ya mara mbili ya kivuko cha MV. Kazi.”

Chuo cha Teknolojia cha India kuanzishwa nchini Tanzania

Ameongeza kuwa kivuko kinapojengwa kinaweza kudumu kwa miaka 30, hivyo kila baada ya miaka mitatu hadi mitano vinapaswa kufanyiwa ukarabati mkubwa, akifafanua kuwa ukarabati mkubwa ulifanyika mwaka 2016 na sasa unakwenda kufanyika ili kusaidia kivuko kudumu na kufikia miaka hiyo 30.

King’ombe amewasisitiza abiria hasa wenye magari katika kipindi ambacho kivuko hicho kitakuwa kwenye ukarabati kutumia njia mbadala ikiwemo kutumia njia ya darajani [Daraja la Nyerere] njia ya Kijichi na Kongowe ili kuepusha usumbufu wa usafiri.

Send this to a friend