Ufafanuzi wa TRA kuhusu kukamatwa mzigo wa Mama Bonge wa Kariakoo

0
49

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema tuhuma zilizotolewa kwa Serikali kuwa ilikuwa inakusanya kodi kwa kutumia mabavu eneo la Kariakoo kwa mfanyabiashara Salome Mgaya maarufu kwa jina la Mama Bonge, zoezi hilo lilikuwa ni ukamataji wa shehena za vitenge zilizoingizwa nchini kwa njia ya magendo.

TRA imefafanua kuwa imekuwa ikifuatilia tuhuma zilizokuwa zikitolewa dhidi ya mfanyabiashara huyo ambapo hivi karibuni uchunguzi wao ulibaini kuwa kulikuwa na makasha mawili yenye mizigo ambayo nyaraka zake zilionesha kuwa bidhaa zilizokuwa ndani yake zilikuwa ni mashuka zilizokuwa zikielekea Chitipa Mzuzu nchini Malawi.

Mamlaka imeongeza kuwa bidhaa hizo hazikuwa mashuka kama ilivyoorodheshwa kwenye nyaraka bali zilikuwa ni vitenge vilivyotarajiwa kuingizwa nchini pasipo kulipiwa kodi ambazo zilihusishwa na mfanyabiashara huyo.

Utafiti: Jeshi la Polisi lashika namba 1 kwa rushwa nchini

Kwa mujibu wa TRA imesema baada ya Kikosi cha Kuzuia Magendo kwa kushirikiana na Askari Polisi kufika eneo la Tabata Matumbi ambapo shehena hiyo ilikuwa ikishushwa na kuthibitika kuwa ni marobota 290 ya vitenge na sio mashuka, Mama Bonge alijitokeza na kukiri kuwa mzigo huo ni wa kwake.

Aidha, TRA imesema inawahakikishia wafanyabiashara na Watanzania kuwa itaendelea kukusanya kodi kwa weledi kama ilivyoelekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na kutoa onyo kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na vitendo vya ukwepaji kodi.

Send this to a friend