Uganda: Dereva bodaboda ajiua kwa kujichoma moto ndani ya kituo cha polisi
Dereva bodaboda mwenye umri wa miaka 29 amefariki dunia baada ya kujichoma kwa moto akiwa ndani ya kituo cha polisi nchini Uganda baada ya polisi kukataa kuachia pikipiki yake.
Pikipiki ya Hussein Walungembe ilikamatwa wilayani Masaka ikiwa ni utekelezaji wa zuio la pikipiki kupakia abiria ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, ambapo pikipiki zimeruhusiwa kubeba mizigo tu.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, Walungembe alimuazimisha rafiki yake pikipiki hiyo ambaye alikamatwa akiwa amebeba abiria, na Walungembe alipofika kituoni mara kadhaa kutaka pikipiki yake iachiliwe hakufanikiwa.
Alhamisi Julai 2 mwaka huu alijifungia ndani ya chumba kwenye kituo hicho na kujichoma moto kwa kutumia petroli iliyokuwa kwenye chupa ya maji.
Mbali na kifo hicho afisa mmoja wa polisi alijeruhiwa pamoja na nyaraka na vifaa vingine viliharibiwa.
Hata hivyo baadhi ya madereva wameeleza kuwa maafisa wa polisi walikuwa wakitaka rushwa TZS 92,000 ($40) ili kuiachia pikipiki hiyo.
Kufuatia tukio hilo Msemaji wa Jeshi la Polisi, Paul Kangave amesema kuwa tayari uchunguzi umeanza kuweza kubaini hasa kilichotokea.