Uganda inavyokabiliwa na changamoto ya kifedha kukamilisha mradi wa SGR, Eacop

0
20

Katika hatua kubwa ya maendeleo, Uganda imeingia makubaliano na kampuni ya Kituruki, Yapi Merkezi, kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) kutoka Malaba hadi Kampala.

Mkataba huo wenye thamani ya dola bilioni 2.9 umetia matumaini kwa taifa hilo baada ya kusubiri kwa miaka 16, ambapo ujenzi huo utawezesha reli hiyo kubeba mizigo kwa haraka zaidi, hivyo kusaidia kuboresha uchumi wa nchi kupitia usafirishaji wa bidhaa kwa gharama nafuu.

Aidha, wakati sherehe za kusainiwa kwa mkataba huo zikiendelea, Waziri wa Nishati wa Uganda, Ruth Nankabirwa ambaye alikuwa akihudhuria mkutano wa Nishati Cape Town, ametangaza kucheleweshwa kwa ufadhili wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (Eacop) kutokana na changamoto za kifedha.

Mradi huo ambao unamilikiwa na Shirika la Mafuta la Uganda, TotalEnergies, CNOOC ya China, na Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania unaendelea kukumbwa na changamoto za kifedha kufutia kuisha kwa mtaji wa wanahisa.

Kwa sasa, ujenzi wa reli ya SGR yenye urefu wa kilomita 273 unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka minne, bila kuwepo benki yoyote inayofadhili mradi huo moja kwa moja, huku Serikali ikipanga kuzindua ujenzi wa reli hiyo rasmi wiki ya kwanza ya Novemba.

Katika mwaka huu wa fedha, serikali imetenga dola milioni 40.8 [TZS bilioni 111.2] kwa ajili ya fidia kwa watu waliopata athari kutokana na mradi wa reli hiyo.

Canon Perez Wamburu, Mratibu wa Kitengo cha SGR Uganda, amebainisha kuwa bajeti kamili ya fidia inakaribia dola milioni 49 [TZS bilioni 133.5], na Wizara ya Fedha imechagua Benki ya Marekani ya Citi Bank kufadhili mkopo wa takriban dola bilioni 3 [TZS trilioni 8.2] ili kufanikisha mradi huo.

Ushindani na Tanzania na Kenya

Uganda iko chini ya shinikizo kutoka kwa majirani zake Tanzania na Kenya, ambazo tayari zimekamilisha mifumo yao ya reli ya SGR. Ili kuhakikisha mtandao wa reli unafanya kazi kwa ufanisi wa kikanda, Uganda inalazimika kujenga sehemu yake ya reli ili kuunganisha na zile za majirani zake.

Kenya pia inafanya juhudi za kuongeza reli yake kutoka Naivasha hadi Kisumu na kisha Malaba, hatua itakayounganisha moja kwa moja na mfumo wa Uganda.

Send this to a friend