Uganda yaanza kampeni ya kufuta majina ya kikoloni na sanamu kwenye mitaa

0
39

Wakati hali ikianza kurejea kuwa shwari nchini Marekani kufuatia maandamano ya kupinga kuuawa kwa raia mweusi, George Floyd, wimbi jingine limeibuka barani Afrika ambapo wananchi wanashinikiza kufutwa/kuondolewa kwa majina yaliyowekwa na wakoloni kwenye mitaa, alama (landmarks) pamoja na maeneo mengine.

Nchini Uganda zaidi ya watu 5,000 wametia saini azimio linaloshinikiza mamlaka husika zibadili majina ya wakoloni kwenye mitaa, alama, sanamu jijini Kampala.

Wapiga kampeni hiyo iliyoanza Juni 9 mwaka huu wamesema kuwa watapeleka azimio hilo bungeni ili iweze kufanyiwa kazi. Wakieleza lengo lao wamesema kuwa wakoloni hawastahili heshima hiyo kwani walikuwa wakatili dhidi ya wazawa.

Miaka 60 baada ya uhuru baadhi ya vitu nchini Uganda bado vina majina ya wakoloni ikiwemo barabara za Major-General Henry Colville na Lord Frederick Lugard zenye majina ya wanajeshi wa Uingereza.

Hii sio mara ya kwanza kuwepo vuguvugu la kubadili majina ya kikoloni nchini humo kwani katika kipindi cha utawala wa Idi Amin (1971-1979) mitaa mingi ilibadilishwa na kupewa majina ya watu weusi ikiwemo Malcom X na Rais Kwame Nkurumah.

Hata hivyo uamuzi huo ulikumbana na vikwazo mbalimbali ambapo Uingereza ilikata uhusiano wake na Uganda, hatua ambayo ilipelekea baadhi ya majina kurejeshwa kwani ilionekana yamebadilishwa kinyemela kwa sababu hakukuwa na bunge.

Wakati hayo yakiendelea nchini Uganda, Meya wa Jiji la Dakar, nchini Senegal amesema kuwa atashinikiza kubadilishwa majina ya mitaa na alama nyinginezo zenye majina ya wakoloni.

Send this to a friend