Wizara ya Afya nchini Uganda imethibitisha kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola katika Mji mkuu Kampala, huku mgonjwa wa kwanza aliyethibitishwa akifariki kutokana na ugonjwa huo.
Mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 32 ambaye ni muuguzi katika hospitali ya rufaa ya Mulago jijini humo, kabla ya umauti alipewa matibabu katika vituo mbalimbali ikiwemo Mulago baada ya kupata dalili za homa, maumivu ya kifua na shida kupumua.
“Mgonjwa huyo alipatwa na matatizo mengi ya kiafya na akafariki dunia katika hospitali ya rufaa ya Taifa ya Mulago Januari 29. Sampuli za baada ya kifo zilithibitisha kuwa alikuwa na aina ya ugonjwa wa Ebola ya Sudan (strain),” imesema Wizara.
Uganda iliwahi kukumbwa na mlipuko huo mwishoni mwa mwaka 2022, na mlipuko huo ulitangazwa kuisha Januari 11, 2023 baada ya kufanya jitihada za kudhibiti maambukizi ya virusi.
Mlipuko huo uliua watu 55 kati ya 143 walioambukizwa na waliofariki ni pamoja na wafanyikazi sita wa afya.