Ugonjwa wa ajabu wazuka India, mtu mmoja afariki

0
36

Mtu mmoja amefariki dunia na wengine zaidi ya 200 wamelazwa hospitali kutokana na ugonjwa ambao haujafahamika uliozuka katika jimbo la Andhra Pradesh, Kusini mwa India.

Madaktari wamesema watu walioshikwa na ugonjwa huo wanaonesha dalili mbalimbali ikiwa ni pamoja na kichefuchefu, kukosa nguvu na kuzimia.

Uchunguzi unaendelea juu ya ugonjwa huo ambao umekumba wakazi wengi wa eneo la Eluru mwishoni mwa wiki.

Ugonjwa huo umekuja wakati Taifa hilo likikabiliana na maambukizi ya virusi vya corona (COVID19), ikiwa ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi baada ya Marekani.

Hata hivyo vipimo vimeonesha kuwa wagonjwa hao hawana maambukizi ya #COVID19.

“Watu wote waliougua, hasa watoto, walianza kutapika mara tu baada ya kuelezea kuwa na maumivu machoni. Baadhi yao walizimia,” afisa wa afya kutoka hospitali ya serikali eneo la Eluru ameliambia gazeti la The Indian Express

Hadi sasa watu 70 wameruhusiwa kutoka hospitalini huku wengine 157 wakiendelea na matibabu.