Uhamiaji yapewa siku 60 kesi ya uraia ya bosi wa Twaweza au irudishe pasipoti yake

0
18

Mahakama ya Rufani imesema kitendo cha Idara ya Uhamiaji Tanzania kushikilia hati ya kusafiria ya Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja bila kukamilisha uchunguzi na wala kumpa taarifa kuhusu maendeleo ya uchunguzi huo ni ukiukwaji wa haki zake.

Mahakama imesema hayo leo wakati ikitoa uamuzi wa rufani iliyofunguliwa na upande wa utetezi ukipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi yake aliyokuwa akiiomba mahakama hiyo iiamuru Idara ya Uhamiaji pamoja na mambo mengine imrejeshee hati yake.

Mbali na kusema hayo, Mahakama ya Rufani imeipa Uhamiaji siku 60 kukamilisha uchunguzi wa kesi hiyo, na endapo wakishindwa kukamilisha wamrejeshee Eyakuze hati yake.

Aidha, mahakama imesema endapo hati hiyo itakuwa imekwisha muda wake, idara hiyo imuwezeshe kupata hati mpya.

Mahakama imeeleza kuwa licha ya kwamba sheria haijaweka ukomo wa muda wa uchunguzi, uchunguzi wa uraia wa Eyakuze kuchukua zaidi ya mwaka mmoja wakati nyaraka za kuthibitisha uraia wake zinaweza kupatikana kwa mshitakiwa, si sahihi.

Idara ya Uhamiaji ilimuamuru Eyakuze awasilishe hati yake ya kusafiria kwa maofisa wa idara hiyo Julai 24, 2018, kwa madai kwamba wanachunguza uraia wake baada ya kupokea taarifa za utata wa uraia wake.

Send this to a friend