
Uingereza imetangaza kusitisha baadhi ya misaada yake ya kifedha kwa nchi ya Rwanda pamoja na kuweka vikwazo vya kidiplomasia kwa serikali ya Rwanda, kutokana na madai ya kuhusika kwake katika mgogoro wa kijeshi mashariki mwa DRC.
Hatua hiyo imekuja wakati Rwanda inazidi kukabiliwa na shinikizo la kimataifa kufuatia tuhuma kuwa inaunga mkono kundi la waasi la M23, ambalo tangu Januari limechukua udhibiti wa maeneo muhimu yakiwemo miji mikubwa ya Goma na Bukavu pamoja na maeneo tajiri kwa rasilimali za madini.
Hatua hizo ni pamoja na kusitisha ushiriki wa maafisa wa ngazi za juu kwenye hafla zinazoandaliwa na serikali ya Rwanda, kupunguza shughuli za kukuza biashara na Rwanda, na kusitisha msaada wa moja kwa moja wa kifedha kwa serikali ya Rwanda, isipokuwa kwa miradi inayosaidia watu maskini na walio katika mazingira magumu zaidi.
Ingawa Kigali inakanusha kuhusika moja kwa moja na kundi hilo, inasisitiza kuwa vikosi vyake vya ulinzi vimekuwa vikichukua hatua za kujihami dhidi ya makundi yenye uhasama yanayojificha ndani ya DRC.
Katika taarifa rasmi, serikali ya Uingereza ilieleza kuwa itaendelea kufuatilia hali hiyo na haitarejesha ushirikiano wa kawaida na Rwanda hadi pale kutakapokuwa na maendeleo ya kweli katika kusitisha mapigano na kuondolewa kwa majeshi ya Rwanda kutoka ardhi ya Congo.