Uingizwaji dawa za kulevya nchini wapungua kwa 90%

0
40

Tanzania imefanikiwa kupunguza uingizwaji wa dawa za kulevya kwa asilimia 90 kufuatia jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali za  kupunguza tatizo la dawa za kulevya nchini.

Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema kuwa tatizo la dawa za kulevya katika jamii ni suala mtambuka linalohitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kupambana nalo wakiwemo waathirika wa dawa za kulevya na jamii kwa ujumla, ambapo Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kukabiliana nalo.

“Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2019 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya dawa za kulevya na uhalifu (UNODC), nchi yetu ilifanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kwa asilimia 90. Pia, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imeshinda kesi za wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya pamoja na kuwakamata wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Aidha,  kwa kipindi cha miaka mitano kutoka mwaka 2015 hadi  Juni, 2020, jumla ya kg 188,489.93 za bangi, kg 124,080.33 za mirungi, kg 58.46 za cocaine, na kg 635.57 za heroin, zimekamatwa pamoja na  jumla ya watuhumiwa 73,920 walikamatwa,” alisema Waziri Mhagama

 Aliongeza kuwa Mamlaka hiyo imefanikiwa kufanya ukaguzi katika kampuni 167 zinazojihusisha na uingizaji wa kemikali bashirifu, sambamba na kukamata kiasi cha lita za ujazo 480,000 na kg 22,145 za kemikali bashirifu zilizoingia nchini bila ya kufuata utaratibu.

Waziri Mhagama ametaja mafanikio mengine ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kuwa ni kupanua huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya nchini, ambapo kumekuwa na ongezeko la vituo sita na hivyo kufanya jumla yake kuwa vituo nane hadi kufikia machi 2020 vikihudumia waathirika 8,500 kwa siku kutoka vituo vitatu vilivyokuwa vikihudumia waathirika 3,500 mwaka 2016.

Vilevile, Mamlaka imekuwa ikisimamia upatikanaji wa uhakika wa dawa ya methadone kwa ajili ya tiba ya waraibu wa heroin kwa kusimamia uagizaji, usambazaji na udhibiti wake, kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa na Kikanda katika mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya na uhalifu wa kupangwa kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Taifa linaloshughulikia masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) pamoja na Taasisi nyingine za Kimataifa.

“Tatizo la dawa za kulevya linavuka mipaka ya nchi yetu, hivyo ushirikiano umeelekezwa zaidi katika kubadilishana taarifa za kiintelijensia na operesheni za pamoja. Ambapo mwaka 2019 nchi yetu iilisaini mkataba na nchi za Msumbiji na Afrika ya Kusini juu ya udhibiti wa usafirishaji wa dawa za kulevya katika njia ya kusini kwa kuwa wafanyabiashara wengi wakubwa wamehamia katika nchi hizo baada ya udhibiti kuwa mkali nchini” alisisitiza Waziri Mhagama

 Aidha, Waziri Mhagama  aliitaka jamii kuendeleza ushirikiano wa kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya kwa kuwa tatizo hilo ni  suala mtambuka na linahitaji ushirikiano kutoka katika taasisi za Serikali, Kiraia, Kimataifa na jamii yote kwa ujumla, na hivyo jamii ijenge uelewa sahihi wa tatizo la dawa za kulevya ili kuimarisha mapambano dhidi yake.

Wiki hii Tanzania inaungana na mataifa mbalimbali duniani katika kuadhimisha Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani huku  kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa Tujenge Uelewa sahihi wa Tatizo la Dawa za Kulevya ili kuimarisha mapambano dhidi ya Tatizo hilo.

Send this to a friend