Ujenzi Daraja la JP Magufuli (Kigongo – Busisi) wafikia 47.3%

0
23

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umesema ujenzi wa Daraja la JP Magufuli linalojulikana pia kama Daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2 liko mbioni kumalizika.

Akizungumza Msimamizi wa TANROADS mkoa wa Mwanza, Pascal Ambrose amesema wahandisi wanafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unafikia lengo la kukamilika Februari, 2024.

“Ujenzi sasa uko katika asilimia 47.3 na ukikamilika, mradi utakuwa chachu ya kupunguza umaskini na kuchochea ukuaji wa uchumi katika eneo kubwa,” amesema Ambrose.

Aidha, amesema ujenzi wa daraja hilo ambao utachukua nafasi ya vivuko na kuwa kiungo muhimu kati ya mkoa wa Mwanza na nchi jirani za Rwanda, Burundi na Uganda, utasaidia kupunguza msongamano wa magari kwenye kivuko, utapunguza muda wa usafiri na kuboresha usafiri wa umma.

“Daraja hilo lenye uwezo wa tani 180 litaruhusu magari 1,600 kupita kwa wakati mmoja na kusababisha Mwanza kuwa kitovu kikuu cha biashara Kanda ya Ziwa,” ameongeza.

Ujenzi wa daraja la Kigogo-Busisi ulianza Februari 2020 na linatarajiwa kukamilika Februari 24, 2024.

Ujenzi huo umeshatoa ajira 801 na kati ya hao wazawa ni 745 sawa na asilimia 93, huku wafanyakazi wa kigeni wakiwa 56 sawa na asilmia 7.