Waziri wa Nishati, January Makamba amesema ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2,115 umefikia asilimia 67.
Makamba ameeleza hayo mbele ya wajumbe wa bodi ya TANESCO, wahariri na wanahabari waliotembelea mradi huo kujionea hatua iliyofikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo alibainisha kwamba mafanikio ya ujenzi huo unatokana na ujenzi kufanyika usiku na mchana.
“Kasi kubwa ya ujenzi inaendelea katika mradi huu. Sasa hivi kazi inafanyika saa 24 usiku na mchana. Mtakuwa mashahidi leo [juzi] sikukuu ya Nanenane lakini watu wapo kazini na wanabadilisha zamu tu,” amesema.
Sababu nyingine aliolezea waziri ni maboresho na mabadiliko yaliyofanyika katika menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na bodi yake ambazo zimekuwa zikifuatilia ujenzi wa bwawa hilo na kuwasimamia makandarasi kwa ukaribu.
“Ukitazama maendeleo ya mradi, miaka miwili na nusu ya mwanzo toka Disemba 2018 mpaka June 2021, tulifikia asilimia 37, leo tuko asilimia 67 (ongezeko la takriban mara mbili chini ya mwaka mmoja). Ni kasi kubwa katika kipindi kifupi,” ameongeza.