Ujenzi wa kituo cha afya wamfuta machozi ya kufiwa na Mjukuu wake

0
16

Mkazi wa Kata ya Lilambo, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Juma Msangi amesema fedha zaidi ya TZS milioni 700 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan zimebadilisha taswira ya upatikanaji wa huduma za afya katika halmashauri hiyo, kwa sababu awali walilazimika kufuata huduma mbali.

Amesema kabla ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Lilambo walikuwa wanakwenda umbali wa kilomita hadi Mji Mwema, na kuwa kama upo shambani, likatokea tatizo hadi ufike nyumbani na uanze kutafuta usafiri ni changamoto kubwa. Pia amesema walikuwa wakitumia gharama kubwa ya kusamfirisha mgonjwa hadi Mji mwema.

“Mwaka 2013, mwanangu wa kwanza alikuwa mjamzito, alishikwa na uchungu wakati huo sikuwa nyumbani, iliwalazimu kukodi gari lakini halikuwa imara iliharibika njiani. Wakati nafuatilia niliwakuta njiani mwanangu akiwa hoi baada ya presha  huku mapigo ya moyo ya mtoto yalishuka.

Tulifanikiwa kumfikisha hospitali na kujifungua, ambapo ilibainika mtoto alikuwa amechoka huku mama yake akiwa hoi. Mtoto aliwekewa mashine ya kupumua, haikuchukua muda mrefu akafariki dunia mtoto, nina uhakika endapo tungewahi hospitali tungeokoa maisha ya mjukuu wangu,” amesema Msangi.

Mtendaji wa Mtaa wa Lilambo, Mary Sagimba amesema kituo hicho, kitakuwa na faida kubwa kwa wananchi wa kata hiyo, yenye wananchi zaidi ya 15,000 wanaotoka katika mitaa nane ambayo haina kituo cha afya.

“Huduma za mama na mtoto, upasuaji, jengo la wagonjwa wa nje na matibabu mengine kwa ngazi ya juu yatapatikana hapa,” amesema Mary.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa, Dkt. Frederick Sagamiko amesema “Rais Samia amefanya mambo makubwa ndani ya muda mfupi kwenye halmashauri hii, na siku za mbeleni huenda ikiwa jiji kutokana na maboresho makubwa ya miundombinu yanayoendelea kufanyika.”

Send this to a friend