Ukweli kuhusu suala la Mnyika kumuomba Mangula asaidie Mbowe kuachiwa huru

0
38

Viongozi wakuu wa vyama vya siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia  Tanzania (TCD) wamemuomba Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula kusaidia kuachiwa huru Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

Taarifa kutoka ndani ya kikao cha TCD kilichoifanyika wiki iliyopita  zinaeleza kuwa hatua hiyo ilifikiwa baada ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika kuwasilisha  hoja maalum kwa viongozi hao kujadili suala la Mbowe.

“Bila kuingilia uhuru wa mahakama naomba nilete hoja hii kwenu. Kwa upande mmoja suala hili linaonekana ni CHADEMA, lakini kwa upande mwingine linatuhusu sote. Mheshimiwa Mbowe ni kiongozi mwenzetu na kama sio matatizo aliyonayo hakuna shaka tungekuwa naye kwenye kikao hiki, hivyo suala lake ni letu sote. Naomba tulijadili na ikiwapendeza tuchukue hatua ya kuona tunavyoweza kumsaidia,” alisema Mnyika.

Baada ya wasilisho hilo wajumbe kwa kauli moja walimuomba Mzee Mangula kulichukua suala hilo na kulifikisha kwenye mamlaka za juu ndani ya serikali.

Akizungumza katika kikao hicho mjumbe kutoka NCCR-Mageuzi, Anthony Komu alisema kwamba matatizo ya kisiasa humalizwa kwa mazungumzo. Amesisitiza kwamba ni lazima kuangaliwa kwa namna ya kumaliza mambo hayo ambayo ameeleza hayana afya kwa Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF, Prof.Ibrahim Lipumba alisema kesi ya Mbowe haina mashiko na haiisaidii CCM  wala Taifa, huku akiongeza kuwa kinachofanyika ni kumjenga Mbowe imara wa mwaka 2025.

Baada ya hoja za wajumbe mbalimbali Mangula aliahidi waliyoyasema yatafikishwa kunakohusika ili uchambuzi ufanyike na ionekane namna ya kulishughulikia.

“Hiki hapa ni kitabu cha kesi nzima, kitasaidia katika kazi ya uchambuzi wa kesi hii. Na tangu kesi kuanza kuna watu wameandika mwenendo mzima wa ushahidi, wanaweza kuanzia hapo, alisema Mnyika akimkabidhi Mangula kitabu.

TCD kwa sasa inaundwa na CCM, CUF, CHADEMA, ACT Wazalendo na NCCR Mageuzi.

Mbowe na wenzake watatu, Mohamed Ling’wenya, Adam Kasekwa na Halfan Bwire wanashtakiwa kwa madai ya kupanga njama za kufanya ugaidi na kufadhili vitendo vya ugaidi.

Chanzo: Raia Mwema

Send this to a friend