Rais Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemteua Uledi Abbas Mussa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kwa kipindi cha miaka mitatu (3).
Taarifa ya Ikulu imeeleza kwamba Mussa ni Katibu Mkuu Mstaafu na Mshauri Binafsi wa Masuala ya Kiuchumi wa Kimataifa (GFA Consulting Group), tawi la Tanzania.
Mussa anachukua nafasi ya Dkt. Suleiman Magesa Misango ambaye ataendelea na majukumu yake ya Ukurugenzi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Machi 15, 2017 aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Magufuli alitengua uteuzi wake na kumsimamisha kazi wakati huo akiwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge).
Hatua hiyo ilichukuliwa ili kupisha uchunguzi zaidi dhidi yake kutokana kuwapo kwa tuhuma za kutozingatiwa kwa taratibu zinazotakiwa katika kushughulikia masuala ya uwekezaji.