Ulega akutana viongozi wakuu wa kampuni kutoka China kujadili miradi inayosua sua

0
10

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amekutana na viongozi wakuu wa kampuni kutoka China zinazosimamia miradi ya ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT), madaraja pamoja na barabara hapa nchini kwa lengo la kutafuta suluhisho la miradi inayosua sua kukamilika.

Mazungumzo ya waziri huyo na viongozi hao yamefanyika katika Ofisi za Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) jijini Dar es Salaam ambapo pande zote mbili zimefikia makubaliano kuhusu maendeleo ya miradi hiyo.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Waziri Ulega amesema mkutano huo ni mwendelezo wa hatua alizochukua baada ya ziara yake ya Machi 4, 2025, ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya BRT4 na kupelekea wakandarasi waliokuwa eneo la mradi kukwama na kushindwa kutoa majibu ya msingi kuhusu ucheleweshaji wa kazi, jambo lililopelekea kuitwa kwa viongozi wakuu wa kampuni hizo kutoka makao makuu yao nchini China.

“Tuna furaha kuwa leo viongozi wa kampuni hizo wamefika Tanzania na tumepata nafasi ya kuzungumza nao. Wameeleza changamoto zao, ingawa hazilingani na muda mwingi uliopotezwa. Hata hivyo, tumeweka ahadi mpya za kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa,” alisema Waziri Ulega.

Katika kikao hicho, makampuni mbalimbali yamefanya ahadi za kimaandishi kwa serikali kuhusu ukamilishaji wa miradi. Miongoni mwao ni kampuni ya Shandong, inayotekeleza ujenzi wa miundombinu ya BRT kutoka Mwenge hadi Tegeta.

Kampuni nyingine ni China Geo Corporation (CGC), inayojenga barabara ya kutoka Katikati ya Jiji hadi Mwenge na Mwenge hadi Ubungo kupitia barabara ya Sam Nujoma.

Send this to a friend