Ummy: Tatizo la jinsi mbili linatibika, msiwafiche watoto

0
26

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa wito kwa Watanzania kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye jinsi mbili bali wawapeleke hospitali ili waweze kupata huduma mapema.

Amesema hayo Juni 6, 2024 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa tatu wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji Urolojia Tanzania (TAUS) unaofanyika Jijini Dar Es Salaam, ambapo ameeleza kuwa wazazi wanapaswa kuwapeleka watoto wao hospitali mapema kwa ajili ya upasuaji kwani tatizo hilo linatibika.

Aidha, Waziri Ummy amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha matibabu katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kuwa nchi ya kutembelewa kwa ajili ya tiba utalii.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameanzisha programu maalumu iitwayo Dkt. Samia Super-Specialized Scholarship Program ya ufadhili wa wataalam wa ubingwa bobezi ambapo katika mwaka wa Masomo 2023/2024, jumla ya Shilingi bilioni 10.9 zilitengwa kwa ajili ya ufadhili wa wanafunzi 1,109 kwa ajili ya masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi,” amesema.

Amesema, kati ya wanafunzi hao 1,109 wanafunzi 33 watakwenda kusomea ubingwa bobezi kwa ongezeko la wanafunzi 26 sawa na asilimia 37 ikilinganishwa na mwaka wa masomo wa 2022/2023 ambapo kulikuwa na wanafunzi 7 wa ubingwa bobezi.

Send this to a friend