Umoja Party yaeleza sababu ya kutumia picha ya Magufuli

1
27

Mwanzilishi wa Chama cha Umoja Party, Seif Maalim ametoa sababu za kwanini chama hicho kinatumia picha ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika fulana zao.

Akizungumza na Gazeti la Mwananchi hapo jana, Maalim alisema chama hakina nia mbaya kutumia picha hiyo kwa kuwa ni moja ya njia ya kujitangaza kwa wananchi.

“Unajua sera zetu zinaendana mrengo wa falsafa za yule anayeonekana katika picha (Hayati John Magufuli) kwenye fulana. Ni harakati za kujitangaza kwa wananchi na hatuna nia mbaya. Kama ni kosa kisheria basi tupo tayari kujirekebisha,” amesema.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, ilidai kuwa Umoja Party imewasilisha maombi ya usajili wa muda na mchakato bado unaendelea lakini chama hicho kimekuwa kikikiuka utaratibu wakati maombi yao yakishughulikiwa.

Ameongeza kuwa, kuna picha zinasambaa mtandaoni zikionesha watu wanaonekana kuwa wanachama na wamevalia fulana zenye bendera ya chama hicho pamoja na picha ya kiongozi ambaye si mwanachama wao.

“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatumia fursa hii kuwakumbusha wanaotengeneza, wanaovaa fulana hizo na Watanzania wote kuwa, ni kosa la kisheria kwa taasisi yoyote kufanya kazi kama chama cha siasa wakati sio chama cha siasa kilichosajiliwa,” ameeleza

Kiongozi wa chama hicho aliishukuru ofisi ya msajilli kwa maelekezo yao na kuahidi kuwa wapo tayari kurekebisha makosa yao kwa kuwa chama hicho kinatii sheria na taratibu za nchi.

Send this to a friend