Tanzania imepokea msaada wa Euro milioni 166 (sawa na takribani TZS bilioni 380) kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mitatu ikiwemo kuibua fursa zitokanazo na bahari (uchumi wa buluu), sekta jumuishi ya fedha na kuimarisha ushirikiano.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema msaada huo umeidhinishwa na Umoja wa Ulaya katika mwaka wa pili wa utekelezaji wa ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kwa kipindi cha miaka saba kuanzia mwaka 2021 hadi 2027, ambapo katika awamu ya kwanza Serikali ilipokea msaada wa Euro milioni 180 (sawa na zaidi ya TZS bilioni 400).
Tanzania yapata mkopo wa bilioni 310 kutoka Korea
“Fedha hizi ni sehemu ya matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan, iliyofanyika mwezi Februari, 2022 jijini Brussels, nchini Ubelgiji ambapo Umoja huo ulitangaza kuipatia Tanzania msaada wa kiasi cha Euro milioni 426 (sawa na TZS bilioni 999.44) kwa kipindi cha miaka minne ijayo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini,” amesema Dkt. Nchemba.
Naye Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya Ulaya, Jutta Urpilainen, amesema Tanzania ni mshirika muhimu wa Umoja wa Ulaya ikiwa ni nguzo imara inayounganisha Mashariki na Kusini mwa Afrika, na kuipongeza kwa kujiimarisha katika nafasi ya uchumi wa kati.