Umoja wa Walimu Wasio na Ajira waiomba Serikali iwatazame kwa jicho la pili

0
5

Umoja wa Walimu Wasiokuwa na Ajira Tanzania (NETO) umeeleza masikitiko yake kwa Serikali kuhusu changamoto ya kutopata ajira tangu mwaka 2015 hadi 2023 kutokana na kigezo cha umri, hali ambayo imewaathiri kiuchumi na kijamii.

NETO, ambao ni umoja maalum kwa walimu waliomaliza masomo yao kati ya mwaka 2015 na 2023 lakini bado hawajapata ajira, umeiomba Serikali kutafuta suluhisho la kuwasaidia ili waweze kutumia taaluma yao kwa maendeleo ya taifa.

“Tumeamua kuchukua hatua hii kwa sababu sisi ni wasomi, na hali hii ni changamoto kubwa kwetu. Tumeona ni vyema kupaza sauti ili Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan asikie na kuona namna anavyoweza kutusaidia,” ameeleza mmoja wa wanachama wa NETO,  Agnes Mpundi.

Aidha, NETO imesema kuwa baadhi ya walimu wameingia katika madeni makubwa baada ya kukopa pesa kwa ajili ya kuhudhuria usaili, huku wengine wakilazimika kuuza mali zao kwa matumaini ya kupata ajira. Kutokana na hali hiyo, wengi wameathirika kisaikolojia baada ya kusubiri kwa muda mrefu bila mafanikio.

“Kimsingi, hali zetu kisaikolojia si nzuri. Tunaonekana tupo sawa, lakini ukweli ni kwamba tumevurugwa na hali hii,” mmoja wa wanachama wa NETO ameeleza.

NETO inasisitiza umuhimu wa Serikali kuchukua hatua za haraka ili kutatua changamoto hiyo na kuwapa walimu hao fursa ya kutumia taaluma yao kwa ustawi wa jamii.