Umri wa JPM kigezo cha Urais 2025

0
12

Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli amesema kuwa hawezi kumpendekeza mtu mwenye umri mkubwa kumzidi yeye awe Rais wa Tanzania pindi muhula wake wa pili utakapomalizila mwaka 2025.

Dkt. Magufuli amesema hayo jijini Dodoma na kufafanua kuwa zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania ni vijana, na ndio wapiga kura, hivyo hawezi kupelekea jina la mtu mzee kwenye Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi ili apitishwe kugombea nafasi hiyo.

“… tukapendekeze kwenye ‘central committee’ tuchague Rais anayenizidi umri mimi? … sasa muangalie mimi nina umri gani nitakapomaliza ujipimie kuanzia kwenye umri pale.”

Amesema anajua kuwa jambo hilo linauma, lakini amesema amelazimika kulisema ili watu wajue kabisa wasije wakapoteza fedha zao wakikazana kuwania kupitishwa kugombea urais.

“… kwa hiyo inawezekana umekaa na jirani yako ambaye ndiye atakuwa Rais labda ni kijana zaidi kwa sababu 65% ya Watanzania ni vijana .”

Amesema kuwa Dkt. Hussein Mwinyi alishinda nafasi ya Rais wa Zanzibar kwa sababu yeye ni kijana na wapigakura wengi ni vijana. Dkt. Magufuli ameomgeza kuwa “huwezi ukawapelekea wapiga kura mtu ambaye si saizi yao.”

Dkt. Mwinyi ameweka rekodi visiwani Zanzibar kwa kupata ushindi wa asilimia 76.27, huku Dkt. Magufuli naye akipata ushindi wa asilimia 84.4.

Send this to a friend